Mheshimiwa Noel Emmanuel Kaganda aliwasilisha rasmi Hati za Utambulisho, kwa Mheshimiwa Lee Jae Myung Rais wa Korea Kusini
Tarehe 22 Julai 2026, Mheshimiwa Noel Emmanuel Kaganda aliwasilisha rasmi Hati za Utambulisho kutoka kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa Mheshimiwa Lee Jae Myung, Rais wa Jamhuri ya Korea. Hatua hiyo iliashiria mwanzo rasmi wa utekelezaji wa majukumu yake kama Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Jamhuri ya Korea.
Baada ya hafla hiyo, Mheshimiwa Balozi Kaganda alikutana na Mheshimiwa Rais Lee, akamfikishia salamu za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na kusisitiza dhamira ya Tanzania ya kuimarisha ushirikiano wa kimkakati kati ya nchi hizi mbili katika maeneo ya sayansi, teknolojia, elimu, utamaduni, utalii, uchumi wa buluu, biashara na uwekezaji. Aidha, alieleza utayari wa Tanzania kuendeleza ushirikiano wenye manufaa ya pamoja kwa maendeleo endelevu ya mataifa yote mawili.
Katika hafla hiyo, Balozi Kaganda aliungana na Mabalozi Wateule kutoka Brazil, Colombia, El Salvador, Kazakhstan, Kuwait, Laos na Nigeria, ambao pia waliwasilisha Hati zao za Utambulisho kwa Mheshimiwa Rais Lee.
Balozi Kaganda aliambatana na Mwenza wake, Mheshimiwa Emmanuela Kaganda Mtatifikolo, Mbunge wa Jimbo la Isimani, Mkoa wa Iringa.
Tanzania na Korea zilianzisha uhusiano wa kidiplomasia mwaka 1992, na Tanzania ilifungua Ubalozi wake nchini humo mwaka 2018. Mheshimiwa Kaganda ndiye Balozi wa tatu wa Tanzania katika Jamhuri ya Korea.




